Posts Tagged ‘bungeni’

Bajeti ya upinzani 2011 yafuta posho za wabunge

Thursday, June 2nd, 2011

Boniface Meena
KAMBI ya Upinzani bungeni imetaja vipaumbele sita vya bajeti yake mbadala ya mwaka wa fedha 2011/2012, ikitaka kufutwa kwa posho (sitting allowance), za vikao vyote vya serikali na wabunge.Vipaumbele hivyo vimetangazwa jana, ikiwa ni wiki moja kabla ya serikali kuwasilisha bungeni, Bajeti yake ya mwaka 2011/2012 itakayotangazwa Jumatano ijayo.

 

Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo ameshatangaza vipaumbele 12 vya Bajeti ya Serikali ambavyo ni mara mbili ya vile vya kambi ya upinzani.
Kambi hiyo ya upinzani bungeni imeeleza kuwa katika vipaumbele vyake itaweka msisitizo katika miundombinu, umeme, kuwezesha ukuaji wa sekta za uzalishaji na hasa ukuaji wa uchumi vijijini na kuimarisha utawala bora.
Imetaja kuimarisha usimamizi wa mashirika ya umma na kuboresha maendeleo ya rasilimali watu kwa kuwekeza kwenye ubora wa elimu nchini.

 

Akitaja vipaumbele hivyo mbele ya waandishi wa habari jana, Naibu Waziri Kivuli, Wizara Fedha na Uchumi, Christina Mughwai alisema dhamira ya bajeti hiyo mbadala ni kutoa unafuu wa kodi kwa wananchi maskini na kuhakikisha kuwa anayepaswa kuilipa anafanya hivyo kwelikweli.
Mughwai ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), alisema bajeti hiyo itasomwa bungeni na Waziri Kivuli wa Fedha na Uchumi, Zitto Kabwe.

 

Kuhusu miundombinu


Alisema kuwa bajeti hiyo itaweka msisitizo kwa barabara zote muhimu ambazo hazijaanza kujengwa, ili zianze kuanzia mwaka huu wa fedha wa 2011/2012.

 

Mughwai alisema pia wataweka msisitizo katika upanuzi wa bandari kwa kutumia ushirikiano wa Sekta Binafsi na Serikali (Public Private Partnership- PPP) pamoja na kuimarisha Bandari ya Mtwara.

 

Alisema katika eneo hilo, watasisitiza pia uboreshwaji wa Reli ya Kati ili iweze kufanya kazi ya kusafirisha mizigo na abiria kwa kiwango cha kuridhisha hadi hapo fedha za kujenga reli mpya zitakapopatikana: “Pia Shirika la Ndege la Taifa liongezewe mtaji wa kulifufua, ili liweze kujiendesha kibiashara na kwa ufanisi.”

 

Tatizo la umeme


Kuhusu umeme, Mughwai alisema bajeti ya kambi ya upinzani itapendekeza fedha zipelekwe kwenye miradi mitatu mikubwa na kwamba miradi hiyo ianze mara moja.

 

“Miradi hiyo ni umeme wa makaa ya mawe megawati 1,500 katika Migodi ya Mchuchuma, Ngaka na Kiwira, pia umeme wa gesi (Mtwara Gas Pipeline) megawati 300 kutoka Mtwara, Dar es Salaam hadi Mwanza,” alisema Mughwai.

 

Alisema kambi hiyo pia itapendekeza mradi kabambe wa kusafirisha na kusambaza umeme mijini na vijijini chini ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na Wakala wa Nishati Vijijini (Rea) ufanye kazi kwa nguvu zaidi.

 

Sekta ya uzalishaji


Katika eneola uzalishaji, Naibu Waziri huyo Kivuli wa Fedha na Uchumi alisema wanasisitiza kuboresha miundombinu, upatikanaji wa majisafi na salama ikiwa ni pamoja na kuongeza ubora wa bidhaa za kilimo: “Tutaelekeza rasilimali za kutosha kwenye kukuza uchumi vijijini.”

 

Utawala Bora


Katika kuimarisha utawala bora, alisema kambi yake inataka serikali itenge fedha za kutosha kuwezesha mchakato wa kuandika Katiba Mpya ili Watanzania wote waweze kushiriki katika mchakato huo.

Pia alisema wanataka kuanzishwe kitengo maalumu kwa ufisadi mkubwa (Serious Fraud Office) ndani ya Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) ili kuimarisha utawala bora.Mughwai alisema kuwa wanataka pia mfumo mpya wa kudhibiti mgongano wa maslahi, hasa kwa wanasiasa kutenganisha mgongano wa maslahi katika biashara zao.

 

Alisema wanataka kuanzishwa kwa ofisi ya bajeti ya Bunge ili kuweka uwazi zaidi kwenye Bajeti ya Serikali kwa kuwa hivi sasa wabunge hawahusishwi katika kuipanga: “Tunapendekeza itungwe Sheria ya Bajeti itakayowezesha kuanzishwa kwa Ofisi ya Bajeti.”

 

Maendeleo ya rasilimali watu

 

Waziri huyo Kivuli wa Fedha na Uchumi alisema katika maendeleo ya rasilimali watu, kambi yake inataka kuhakikisha watoto wanaomaliza kidato cha nne, wanapata mafunzo ya ufundi ili waweze kujiajiri wanaporudi vijijini.

 

“Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu inapata fedha za kutosha kutoka kodi ya uendeshaji ujuzi, robo tatu ya kodi hii ambayo inakwenda Hazina ibaki kwenye bodi ili kukidhi mahitaji ya mikopo. Kimsingi lengo la bajeti yetu katika elimu ni kupata elimu bora na si wingi wa majengo ya shule ama wanafunzi wanaomaliza shule.”

 

Naibu msemaji huyo alisema kuwa wapinzani wanataka kuanzishwa pensheni kwa wazee wote wenye umri zaidi ya miaka 60 na kuanzishwa kwa bima ya afya kwa wananchi wote.”Bima hii iwe ni ya lazima kwa watu wote, wafanyakazi na wasio wafanyakazi na ichangiwe na wananchi wenyewe pamoja na serikali,” alisema.

Usimamizi wa mashirika ya umma

 

Kuhusu usimamizi wa mashirika ya umma, alisema kambi ya upinzani inataka uanzishwe Mfuko wa Taifa wa Uwekezaji (National Investment Fund) kwa ajili ya kutoa mitaji kwa mashirika ya umma na mapato yake yatokane na asilimia ya faida za mashirika inayokwenda kwenye bajeti sasa.

 

Alisema kambi hiyo pia inataka kuanzishwa kwa Mamlaka ya Mafuta na kulibadili Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kuwa shirika la kibiashara la mafuta.Pia kambi hiyo inataka kupunguzwa bei ya mafuta kwa asilimia 40 na kupanua wigo wa kodi kwa kuweka lengo la kukusanya mapato ya ndani sawa na asilimia 20 ya pato la taifa.

 

Mughwai alisema kambi ya upinzani pia inataka pia kuangaliwa upya kwa mfumo wa utawala wa kodi akitolea mfano kampuni zinazofanya kazi nchini, lakini zimesajiliwa nje hali inayosababisha zilipe kodi katika nchi zilikosajiliwa na taifa kukosa mapato.

 

“Tunataka kodi inayoitwa ‘Presamptive Tax’ ifutwe kwa sababu inasababisha kampuni ndogo zisijisajili, hii husababisha ukwepaji wa kodi hasa katika sekta isiyo rasmi.Alisema mashirika ambayo serikali ina hisa yajisajili katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), ili ziweze kuuzwa.

 

Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2011/2012 itaelekezwa katika sekta za nishati, elimu, kilimo na mifugo. Sekta nyingine zitakuwa ni za miundombinu,Uvuvi, maendeleo ya viwanda, afya, maji, ardhi, nyumba na makazi, rasilimali watu, sayansi na teknolojia, huduma ya fedha na masuala mtambuka.

 

Chanzo:Mwananchi

Vijana CHADEMA watikisa Bunge

Tuesday, April 19th, 2011

WABUNGE machachari vijana wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) jana waliwasha moto bungeni, huku wakiilazimisha serikali na Bunge kuchukua hatua za haraka kujinusuru.

 

Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, alimbana vilivyo Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, akidai waziri huyo amelidanganya Bunge, huku Mbunge wa Ubungo, John Mnyika, akiibana serikali juu ya ufisadi wa Kagoda.

 

Wakati Lissu alikuwa tayari kuthibitisha kauli yake pale pale, kama kanuni zinavyotaka, Spika wa Bunge, Anne Makinda, aliingilia kati kumnusuru Ngeleja, akataka mbunge huyo awasilishe hoja yake kwa maandishi kuthibitisha uongo wa waziri Ijumaa wiki hii badala ya jana.

 

Hata hivyo, Lissu alipinga uamuzi huo, akitaka kutetea kauli yake na kuthibitisha uongo wa waziri jana hiyo hiyo, bila mafanikio.

 

Lissu hakuridhika na majibu ya Ngeleja yaliyotokana na swali lake la nyongeza.

 

Katika swali hilo, Lissu alitaka kujua hadi sasa ni wananchi wangapi wameondolewa katika kata za Mang,onyi, Ikungi na Mhitiri ili kupisha kampuni ya uchimbaji madini ya Shanta Mining Co. Ltd iliyopewa leseni ya kutafiti dhahabu katika jimbo lake.

 

Vile vile, alitaka kujua kiasi cha pesa walicholipa; kwanini wamejenga uwanja wa ndege, na kwanini kampuni hiyo ilitwaa maeneo mengine kwa nguvu.

 

Waziri Ngeleja alijibu kwa kifupi, akisema kampuni hiyo haijachukua maeneo hayo kwa nguvu, na akaongeza kuwa hata mwaka 2008 alifanya ziara na kushuhudia hali hiyo.

 

Ndipo Tundu alisimama na kutaka kuuliza swali la nyongeza, lakini Makinda alikataa, Lissu akaomba mwongozo wa Spika.

 

Tundu aliposimama, alisema katika majibu yake Ngeleja ni mwongo; na akataka atoe ushahidi kuthibitisha uwongo wa waziri.

 

Hata hivyo, Spika Makinda alimtaka Tundu Lissu kuandika maelezo yake, ili Ngeleja ajibu, na kwamba atafikisha maelezo hayo kwenye vyombo vyake ili wayapitie na kutoa majibu bungeni.

 

Hali hiyo ilimlazimu Tundu kusimama tena na kupambana na Spika kwa kutumia kanuni za Bunge, akihoji iweje Mbunge anapotoa madai kama hayo atakiwe kuthibitisha papo hapo lakini yeye anaambiwa aandike.

 

Akijibu hoja hiyo, Makinda alisema kutokana na muda mchache uliopo, hawezi kuruhusu malumbano hayo Bungeni kwani yatamaliza muda wa maswali na majibu.

 

Alisema mazingira yaliyotokea kwa Tundu, yanafanana na tukio la Mbunge mwingine wa CHADEMA wa Arusha Mjini, Godbless Lema wa Arusha Mjini, ambaye katika mkutano wa Bunge uliopita, alitaka kujua hatua ambayo mbunge anaweza kumchukulia kiongozi mkuu kama Waziri Mkuu iwapo amelidanganya Bunge.

 

Ilikuwa mara baada ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda kutoa kauli ya serikali kuhusu maandamano na mkutano wa CHADEMA, ambayo polisi waliyasambaratisha na kuua watu watatu.

 

’’Jamani tusome vizuri kanuni. Hili ni kama tukio la Lema ambalo nitalitolea majibu kwenye mkutano huu. Sio lazima utoe maoni sasa hivi ndani ya Bunge.

 

“Ninamuagiza Tundu aniandike na Ngeleja atajibu, nitapeleka kwenye vyombo vyangu ambako wanaweza kuwakutanisha Lema na Ngeleja na Bunge kusomewa uamuzi Ijumaa. Huo ndio utaratibu,” alisema Makinda.

 

Hata hivyo hatua hiyo haikumridhisha Tundu Lissu ambaye akiwa nje ya Bunge alisema Spika ana nia ya kuwalinda mawaziri wanapobanwa bungeni.

 

Kwa upande wake, Mnyika aliibua upya suala la ufisadi wa Kampuni ya Kagoda, inayodaiwa kuchota mabilioni ya fedha katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), mali ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ambalo serikali imekuwa anaogopa kulijadili.

 

Mara kadhaa huko nyuma, viongozi waandamizi serikali wamesema kwamba ”kagoda hakamatiki” na kwamba ”hafahamiki,” huku taarifa zikionyesha kuwa ufisadi huo ulifanyika katika mazingira ya kisiasa yanayodaiwa kukinufaisha Chama Cha Mapinduzi (CCM).

 

Baadhi ya watu wanaodaiwa kuchota pesa hizo ni watu wazito ndani ya CCM na mfumo wa utawala nchini.

 

Ufisadi huo uliibuliwa Bungeni na aliyekuwa Mbunge wa Karatu, Dk. Willibrord Slaa, katika Bunge liliopita. Dk Slaa ni Katibu Mkuu wa CHADEMA.

 

Jana Mnyika aligusia suala hilo wakati akiuliza swali la nyongeza, akitaka kujua kauli ya serikali lini itakamilisha uchunguzi kuhusu kampuni hiyo ya Kagoda na kuwachukulia hatua wahusika.

 

Akijibu swali hilo kwa kifupi sana, Waziri wa Nchi Ofisi Rais (Utawala Bora), Mathias Chikawe, alisema serikali bado inaendelea na uchunguzi wa tuhuma dhidi ya kampuni hiyo.

 

Hata hivyo, jibu hilo lilionekana kutowaridhisha wabunge wengi kwani zaidi ya wabunge kumi walisimama kutaka kuuliza maswali ya nyongeza.

 

Akiuliza swali lingine la nyongeza, Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid (CUF), alihoji kuwa kwa kuwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa,(TAKUKURU) Dk. Edward Hosea, alisema tatizo la kesi ya ufisadi mkubwa kama wa Kagoda ni DPP, hivyo alihoji kama Serikali iko tayari kutoa taarifa Bungeni kuonyesha kesi zilizokwama kwa DPP.

 

Akijibu swali hilo, Waziri Chikawe alisema Serikali ipo tayari kutoa taarifa hiyo bungeni na itafanya hivyo katika mkutano huu wa tatu wa Bunge unaoendelea mjini hapa.

 

Kashfa ya Kagoda ambayo ilipata kulitikisa Bunge miaka mitano iliyopita, limekuwa likipigwa danadana na Serikali kwa sababu za kisiasa.

 

Kampuni ya Kagoda ilikwapua jumla ya dola za Kimarekani 30,732,658.82 (Sh. 40 bilioni) katika Akanuti ya Madeni ya Nje (EPA), ndani ya BoT. Fedha hizi na nyingine zipatazo Sh. 73 zilichotwa katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2005.

 

Taarifa zinaonyesha kuwa ni Yusuf Manji aliyedhamini Kagoda kufungua akaunti katika tawi la CRDB Benki la Holland jijini Dar es Salaam ambako mabilioni ya shilingi yalipitia.

 

Serikali imekuwa ikikana kufahamu wamiliki wa Kagoda na kwa zaidi ya miaka mitano sasa imekaa kimya juu ya wizi wa kampuni hiyo.

 

Aidha, serikali imekuwa ikijikanyaga kuhusu wizi huu. Aliyekuwa Waziri wa Fedha, Zakia Meghji, aliwaandikia maodita wa kampuni ya Deloitte & Touche ya Afrika Kusini akisema, fedha za Kagoda zilitumika kwa “kazi za usalama wa taifa.”

 

Katika barua yake ya Septemba 15, 2006, Meghji anasema, “Kama unavyofahamu vema, mamlaka ya serikali huwa na siri, vilevile haja ya kugharamia matumizi ya busara. “Kwa hiyo… malipo ya dola 30,732,658.82 za Marekani yaliyofanywa na BoT kwa Kagoda Agriculture Limited, yaliidhinishwa na serikali kugharamia matumizi yake nyeti na ilikuwa lazima kuchukua hatua hii ya kudumisha usiri huu.”

 

Hatua hii inaleta maswali mengi kuliko majibu; yakiwa ni pamoja na iwapo Manji na wakwapuaji wa Kagoda ndio hasa wanaitwa “Usalama wa Taaifa.”

 

Baadaye jana Mnyika alitoa tamko kwa vyombo vya habari likisema:

 

“Itakumbukwa kwamba Kagoda inatuhumiwa kuchota jumla ya dola za Marekani 30,732,658.82 (Sh. 40 bilioni) katika Akanuti ya Madeni ya Nje (EPA) katika Benki Kuu (BoT) mwaka 2005.

 

“Serikali imekuwa ikijichanganya kuhusu ufisadi wa Kagoda; mathalani tarehe 15 Septemba 2006 Waziri wa Fedha wa wakati huo Zakhia Meghji aliandika barua kwa wakaguzi wa mahesabu wa kampuni ya Deloitte & Touche ya Afrika Kusini kuwa fedha za Kagoda zilitumika kwa kazi ya usalama wa taifa na kutaka usiri na busara katika ukaguzi wa mahesabu ya kampuni hiyo. Baadaye Waziri Meghji alifuta barua hiyo.

 

“Nyaraka mbalimbali zinaonyesha kwamba cheti cha usajili wa Kagoda kilichotolewa na ofisi ya Wakala wa Usajili wa Leseni za Biashara na Makampuni (BRELA) kinaonyesha Kagoda ilisajiliwa 29 Septemba 2005.

 

“Mpaka sasa siri za ufisadi wa Kampuni hiyo na wa kampuni zingine zilizohusika kwa wizi wa Kagoda zimebaki kwa Rais Jakaya Kikwete na wajumbe watatu wa timu uliyoiunda wakati huo ikiwemo idadi na majina ya watuhumiwa wanaodaiwa kurejesha sehemu ya fedha.

 

“Wakati serikali imekuwa ikieleza kwamba haiwajui wamiliki wa Kagoda; taarifa mbalimbali zimekuwa zikimtaja Rostam Aziz (Mb) na wengine.

 

“Baadhi ya vyombo vya habari vimewahi kuandika kwamba Wakili Bhyidinka Sanze wa Kampuni ya mawakili ya Malegesi (Malegesi Law Chambers) ya Dar es Salaam katika maelezo yake kwa Kamati ya Rais ya kushughulikia wizi kwenye akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) alikiri kwamba alishuhudia mkataba wa Kagoda na mikataba mingine iliyohusu ufisadi huo.

 

“Wakili huyo alieleza kwamba mkataba huo ulishuhudiwa na Caspian Construction Limited (inayomilikiwa na Rostam Aziz) iliyopo Dar es salaam na kwamba alielezwa kuwa fedha hizo ni kwa ajili ya kuiwezesha CCM kugharamia uchaguzi na kwamba maelekezo hayo yalitolewa kwa aliyekuwa gavana wakati huo (marehemu Daudi Balali) na Rais wakati huo Benjamin Mkapa.

 

“Hata hivyo, pamoja na serikali kwa wakati wote kuendelea kusisitiza kutowajua wamiliki wa Kagoda; Taarifa za hivi karibuni zimemtaja mfanyabiashara Yusuph Manji kupitia kampuni ya familia yake ya Quality Finance Corporation Limited (QFCL) anadaiwa na serikali kurejesha fedha za Kagoda.

 

“Katika mazingira haya ya utata ndio maana natoa kauli ya kuitaka serikali kutoa tamko la kina kuhusu kashfa hii ya Kagoda.”

 

Swali la msingi liliulizwa na Mbunge wa Viti Maalum Pudenciana Kikwembe (CCM), kuhusu rushwa, akitaka kujua Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba lengo la taifa katika kupambana na rushwa linafanikiwa.

 

Waziri Chikawe akijibu swali hili alisema kwa kuwa watoaji na wapokeaji wa Rushwa ni wananchi wenyewe, hivyo kila mmoja anapaswa kuwa askari.

 

“Vita hii ni yetu sote, ninawaomba viongozi wote wa serikali, siasa na dini na jamii kwa ujumla, kukemea rushwa kila wanapopata nafasi ya kufanya hivyo,” alisema Spika.

 

Wakati huo huo, moto juu ya mjadala wa Katiba mpya uliwaka jana Bungeni, huku baadhi ya wabunge wakitaka muswada wa serikali unaopelekwa Bungeni uahirishwe.

 

Aliyeibua hoja hiyo ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA), akisema wananchi wanahitaji kupewa muda wa kujadili suala hili kabla halijatungiwa sheria.

 

Zitto alisema ni wabunge wapewe fursa ya kuwaelimisha wananchi wao.

 

Lakini Waziri wa Katiba na Sheria, Celina Kombani, alisisitiza kuwa muswada huo utawasilishwa kama ilivyopangwa.

 

Akijibu swali bungeni jana, Kombani alisema kinachofanyika sasa si kupitisha Katiba Mpya bali kuangalia jinsi ya kuunda tume itakayosimamia kutungwa kwa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Mpya.

 

Alisema sheria hiyo, pamoja na mambo mengine, ndiyo itakayoanzisha tume itakayoratibu zoezi la utungwaji wa Katiba Mpya.

 

Alisema muswada huo umekamilika na utawasilishwa katika mkutano huu wa Bunge kwa hatua zaidi.

 

Waziri Kombani ambaye alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum (CUF) Fakharia Shomar Khamis, alisema muswada huo sanjari na kuainisha majukumu ya tume, utaanisha jukumu la utoaji elimu kwa wananchi kuhusu katiba inayotumika sasa.

 

“Watu wanapotosha kwamba Bunge limekuja kupitisha muswada wa Katiba Mpya. Nimeona kwenye kongamano na watu wengine wakijadili. Mkawaambie wananchi hatupitishi katiba mpya sasa,” alisema Kombani.

 

Kwa mujibu wa Kombani, katika utoaji elimu, Serikali itashirikiana na mashirika yasiyo ya kiserikali.

 

Alisisitiza kuwa serikali imeona kuna umuhimu wa kutoa elimu juu ya katiba ya sasa ili wawe katika nafasi nzuri ya kuchangia mawazo ya kuanzishwa kwa Katiba Mpya.

 

Katika swali lake la msingi, mbunge huyo alihoji kama Serikali haioni umuhimu wa kutoa elimu juu ya Katiba ya sasa ili wananchi waweze kuchangia mawazo ya kuanzishwa kwa Katiba Mpya.

 

Hata hivyo, wadau wa katiba, wakiwamo wanasheria, wanasiasa na wasomi kadhaa nchini, wanadai kuwa sheria inayotarajiwa kutungwa kwa muswada huu haikidhi matakwa, na haiendani na mahitaji ya Katiba mpya inayotakiwa.

 

Hoja kuu ambayo imekuwa ikijengwa kwa muda mrefu na wanazuoni, ni kwamba uhalali wa Katiba unatokana na uhalali wa mchakato wa kuitengeneza, na kwamba kwa staili hii ya harakaharaka ya serikali kutunga sheria inayolalamikiwa, wananchi watashindwa kushiriki kutunga katiba yao.

 

Wadau wengi wanadai muswada huu hauna maslahi kwa taifa, bali unalenga kulinda maslahi ya kikundi kinachotawala, na kunyamazisha wakosoaji wake.