Posts Tagged ‘ccm’

RAI YA JENERALI:Hatari ya vurugu inatoka kwa watawala, Slaa asiwape kisingizio

Thursday, June 9th, 2011

Na Jenerali Ulimwengu

 

KATIKA kipindi hiki tunapoikazania Serikali ya Rais Jakaya Kikwete isifanye mchezo na suala la Katiba, tunalo jukumu la kutuliza akili zetu na kupima kwa kina kila tunachokisema na kukiandika.

 

Nasema haya kwa sababu naona kama tunalo tatizo linalotokana na Serikali yetu kuonekana kama vile haina msimamo kuhusu suala hili kubwa na zito. Hakuna dalili za wazi zinazoonyesha kwamba Baraza la Mawaziri limeketi na kulijadili kwa undani na kupata msimamo wa pamoja, na wala hakuna dalili kwamba mkuu wa Serikali hiyo, Rais Kikwete amewapa watu wake maagizo kuhusu nini wafanya na nini waseme kuhusu mada hii ya Katiba.

 

Kinachojitokeza ni taswira ya kuparaganyika kwa mawazo na kutokuelewana miongoni mwa wale wanaotarajiwa kutuongoza. Kwa bahati mbaya, ingawaje sasa naamini watakuwa wamegundua kwamba walichokifikiria kuwa kitu rahisi, ni kigumu kweli kweli na wanatakiwa wajiandae kukishughulikia kwa umakini mkubwa kuliko huo walioudhihirisha hadi sasa.

 

Ningependa nirejee jambo ambalo nimekuwa nikilishadidia kwa muda mrefu kidogo: Suala la Katiba mpya limeshika kasi isiyokuwa ya kawaida, na wala haliwezi kuondoka kirahisi. Linahitaji kufanyiwa kazi itakayowaridhisha wananchi, na hiyo kazi haiwezekani ikafanyika ila kwa kuwahusisha wananchi kwa kiwango kikubwa kinachowezekana.

 

Ukweli ni kwamba, hata kama hatukuwa tumezowea hili, hivi sasa wananchi wanataka mabadiliko makubwa katika maisha yao, na wanataka kuanza na Katiba watakayoiandaa wenyewe.

 

Ni kwa nini wananchi wamefikia kiwango hiki cha utashi, mimi binafsi sina jibu la haraka, na kila mtu anaweza kuwa na maoni yake. Lakini naamini kwamba wananchi wengi wameanza kung’amua kwamba mambo hayaendi kama ambavyo yanatakiwa yaende.

 

Wanayaona maisha yao yakiwa hayana matarajio tena. wanaona hali zao za kiuchumi na kijamii zikizidi kuzorota. Wanaona maisha bora waliyoahidiwa kama ni mzaha wamechezewa. Wanawaona watawala wao kama waongo na wanafiki, wasiojali, wala rushwa na wauza nchi. Hawaamini lo lote linalosemwa na watawala kwani wamekwisha kudanganywa mara nyingi.

 

Sasa wamehamanika na wanataka mabadiliko, tena wanataka mabadiliko makubwa.

 

Nimekuwa nikifuatilia kwa kiasi fulani maandamano na mikutano ya viongozi wa CHADEMA katika mikoa ya Kusini, na nimekuwa nikiangalia maelfu ya watu wanaoshiriki katika maandamano hayo na mikutano hiyo. Ningekuwa mtawala ningeshitushwa na mikusanyiko ile kwa sababu ningetambua kwamba inabeba ujumbe mzito kwangu.

 

Ujumbe unaotoka katika maandamano yale na mikutano ile ni kwamba wananchi wamechoka. Ukiona kaumu ya watu kama tuliyoiona katika miji midogo na ya ‘pembezoni’ kama Sumbawanga wanaandamana na kukaa mkutanoni wakisikiliza kama watotot wa shule wanavyokaa darasani kumsikiliza mwalimu, unajua kwamba kuna kitu kimebadilika katika jamii ya Watanzania.

 

Lakini papo hapo ningependa kutoa angalizo. Kama nilivyowahi kuandika huko nyuma, hii si mara ya kwanza tunashuhudia hamaniko la aina hii la kutaka mabadiliko. Nimeandika kwamba tuliwahi kuona, hapa nchini, hamasa walizozua wanasiasa kama Chistopher Mtikila na Augustine Mrema wakati ule. Watu wengi waliwachukulia hawa kama wakombozi wao. Baadaye bila shaka walikuja kugundua kwamba matumaini yao yalikuwa yamegonga mwamba.

 

Lakini shauku ikiisha kujengeka kwamba hali iliyopo haifai na ni lazima ibadilike, shauku hiyo haiishi kwa sababu manabii waliotarajiwa kufanya kazi ya ukombozi wamedondoka kando ya njia, bali shauku hiyo huhamishwa na jukumu la ukombozi likatafutiwa manabii wengine. Na kwetu ndivyo ilivyokuwa.

 

Kikwete alipoingia madarakani mwaka 2005 shauku hiyo ilikuwa imehamishiwa kwake. Bila shaka mwenyewe atakuwa anakumbuka kwamba ilifika mahali wakati wa kampeni ndani ya CCM ikasemwa kwamba hata kama CCM wasingemchagua yeye kuwa mgombea, angepata kuwa rais kwa kupitia chama kingine cho chote. Hayo yalisemwa na wana CCM na wanachama wa vyama vya upinzani pia.

 

Hili nalisisistiza kwa makusudi mazima: Hizi ni dalili za kuhamanika na kukata tamaa kwa Watanzania wengi. Na hali hii imekuwapo kwa muda mrefu toka utawala wa Rais Ali Hassan Mwinyi hadi ule wa Rais Benjamin Mkapa. Sasa inajirudia katika utawala wa Rais Jakaya Kikwete.

 

Wananchi wengi wanaona mkombozi wao mpya, nabii wao mpya, ni CHADEMA. Wanachosema katika lugha ya miili yao ambayo naiona kupitia televesheni na kupitia magazeti, ni kwamba wakipata fursa ya kupiga kura na uchaguzi ukawa “huru na wa haki” wanaweza (na uwezekano huo ni mkubwa) watapiga kura kuichagua CHADEMA.

 

Sasa, kama tunavyojua, uchaguzi mwingine ni mwaka 2015. Bado tunayo miaka minne hadi tupate fursa nyingine ya kupiga kura. Ni vyema kwa wale wanaotaka kufanya mabadiliko katika utawala wa nchi hii kwa njia mbali mbali wakautumia muda uliosalia kujiandaa kwa ajili ya uchaguzi huo, na wale wanaotaka kuiondoa CCM madarakani wafanye kampeni ya nguvu ya kuwahamasisha wapiga kura kimawazo lakini pia na kuwahamasisha wajitokeza siku ya kupiga kura ili watimize azima yao.

 

Ndiyo maana nilijikuta nikiwa na wasiwasi (wiki chache zilizopita) nilipomsikia Katibu Mkuu wa CHADEMA, Willbrod Slaa akizungumza kama vile anao mpango wa kufanya mabadiliko anayotaka kuyafanya kabla ya uchaguzi ujao. Aliposema kwamba kuiondoa serikali ya Kikwete kabla ya 2015 hautakuwa uhaini anaweza kuwa anasema kweli, kwani uwezekano huo upo.

 

Kwa mfano Bunge linaweza, katika mazingira mahsusi yaliyoainishwa na Katiba, likamshitaki Rais kwa kosa la kuidhalilisha Ofisi yake, na kama akikutwa na hatia likamvua madaraka. Hiyo imeandikwa katika Katiba tuliyo nayo hivi sasa, na wala halina haja ya kusubiri Katiba mpya. Ndiyo maana nasema kwamba anachosema Slaa ni cha kweli kwa maana ya vifungu vya Katiba ya Jamuhuri ya Muungano kama ilivyo leo.

 

Kinachonitia hofu ni kwamba napata hisia kwamba Slaa hakujikita katika vifungu vya Katiba, angalau maelezo niliyoyasoma hayakusema hivyo, jambo ambalo linaweza kuzaa tafsiri kwamba njia mojawapo inayofikiriwa ni kuung’oa utawala wa Kikwete kwa maandamano, kama ilivyokuwa Medani Tahrir.

 

Kama hivyo ndivyo alivyokusudia kusema Slaa, kuna tatizo. Tatizo hilo, kwa mtazamo wangu, linakuwa kubwa zaidi kwa kuangalia matukio ya siku hizi chache zilizopita.

 

Tatizo lenyewe si kwamba haiwezekani kuung’oa utawala uliopo kupitia maandamano na bado kitendo cha kuung’oa kikawa si uhaini. Nchi nyingi zimeshuhudia hilo likifanyika, ikiwa ni pamoja na Indonesia, Philippines, Georgia na sasa Tunisia na Misri. Kilichotokea katika nchi hizo ni mapinduzi ya umma uliosimama na kusema “Utawala huu sasa basi!” Ni mantiki ya mapinduzi kama hayo kwamba yanapofanikiwa walioyaongoza wanakwenda moja kwa moja Ikulu, lakini wakishindwa wanatiwa kitanzi.

 

Ni kwa jinsi hii akina Fidel Castro (Cuba) na Nelson Mandela (Afrika Kusini) walikwenda jela lakini hatimaye waliingia madarakani, lakini Pierre Mulele (Kongo) na Mahjoub (Sudan) walitiwa kitanzi.

 

Naamini kwamba Katibu Mkuu wa CHADEMA alitaka kupeleka ujumbe mzito kwa wakuu wa nchi, lakini kila siku ujumbe unaohusu mambo kama haya hauna budi uandaliwe kwa uangalifu na weledi mkubwa ili usije ukazaa tafsiri zaidi ya moja.

 

Ingekuwa vyema kama Slaa angeonyesha subira katika matamko yake. Hivi sasa watu wengi wanamwangalia kama “rais mtarajiwa.” Angechukua muda kujiandaa kwa umakini mkubwa, hasa wa kuyasoma matatizo ya nchi yetu na kufikiria njia mbali mbali za kuyakabili kuanzia na hili la Katiba ambalo sasa naamini kwamba iwapo atachaguliwa kuwa rais mwaka 2015 ( na nasema hili linawezekana kabisa), atalikuta bado lipo kwa sababu sioni dhamira ya kweli ya kulishughulikia.

 

Akijipa muda wa kujifunza zaidi na kukusanya maoni, na kujenga mitandao ya utafiti itakayowahusisha wataalamu wa kumshauri na kukishauri chama chake, akichukua muda kujadili matatizo ya nchi hii na makundi mbali mbali ya kijamii katika shughuli zao mbali mbali na wakamweleza matatizo yao; naye akajadiliana nao… atakuja kugundua kwamba hakuna muda wa kutosha kwa ajili ya maandalizi hayo.

 

Najua mara nyingi umefanyika uchokozi dhidi ya vyama vya siasa na wanasiasa wa upinzani. Uchokozi huo unafanywa makusudi ili kipatikane kisingizio na wapinzani waweze kushutumiwa kwamba ndio waliodhamiria kuvunja “amani na utulivu” na misemo mingine ya kuchekesha ukiangalia “amani na utulivu” vinavyotawala shughuli za chama-tawala.

 

Kwangu ni dhahiri kwamba kama kuna ghasia kubwa zitakazotokea nchini humu, zitaanzia katika vurugu zinazoendelea ndani ya chama hicho tawala. Hata hivyo, Slaa angejiweka mbali na kila kinachoweza kumfanya yeye ama chama chake waonekane, hata kama si kweli, kwamba wao ndio wanaochochea vurugu.

 

Naandika haya nikijua kwamba sasa kuna hamaniko ndani ya duru za watawala, kwa sababu wanajua wamepoteza nguvu za ushawishi na wanachokiona kwamba kinaweza kuwasaidia ni ushawishi wa nguvu, kama ambavyo wanaonekana kutumia mitulinga isiyokuwa na sababu yo yote alimradi tu waonyeshe kwamba wanazo nguvu, kama vile hatujui kwamba wanazo.

 

Katika kutapatapa wamewaingiza na wakuu fulani wa dini ambao nao sasa wanatoa ‘onyo’ kwa CHADEMA kama vile wamegeuka kuwa idara ya usalama ya serikali au wasemaji wa Jeshi la Polisi.

 

Hali hii inatisha, lakini si mpya. Imetokea kila mahali utawala ulipozeeka, ukapoteza njia, ukasahau hata asili yake, ukapuyanga na kubahatisha, ukababaisha na kubangaiza, ukayumba na kutetereka, ukatekwa na waporaji, ukaendelea kujitutumua kwa kuonyesha ukali wa kijeshi kumbe ndani ya roho yake kiini chake kilikwisha kugugunwa na mapanya-buku kwa muda mrefu. Utawala kama huo unao uwezo mkubwa wa kusababisha maafa kutokana na udhaifu wake.

 

Slaa akae chonjo, apunguze hisia, awe m-rais (presidential). Ajifunze zaidi, kwani kama bado ana nia ya kuwania urais mwaka 2015, kazi iliyo mbele yake ni kubwa. Akumbuke tu kwamba, Rais Jakaya Kikwete alikuwa na (angalau) miaka kumi ya kujiandaa kuwa rais, na hii kumi ni ile tunayoijua sisi.

 

Hata baada ya muda huo wa miaka kumi kupita, na hata baada ya miaka mitano ya kuendesha Serikali, inaelekea bado hajajifunza mambo mengi ya msingi kabisa yanayohusu uongozi na utawala. Slaa afanye hadhari, asije akawa vivyo hivyo.

 

Chanzo: Raia Mwema

 

Kagoda scandal queries resurface in Bunge

Tuesday, April 19th, 2011

 

By Mkinga Mkinga
The Citizen Reporter

Dodoma.

 

Queries over the outcome of the investigation on the involvement of Kagoda Agricultural Company Limited, one of firms named in the Central Bank’s External Payment Areas (EPA) account looting scandal, has resurfaced in the Parliament.

 

This time it was the Ubungo MP (Chadema), Mr John Mnyika, who raised the issues during the question and answer session in the House, challenging the government to state the status of the investigation.The company is alleged to be the single biggest beneficiary of funds looted from the Bank of Tanzania’s (BoT) external payment arrears (EPA) account after receiving dubious payments of more than Sh40 billion.

 

In his supplementary question, Mr Mnyika queried why no action has been taken so far against the company.
“I would like to know the progress on the said investigation on the Kagoda Company, which we were earlier told that it is also involving some international investigation agencies,” the MP asked the minister responsible for Good Governance, Mr Mathias Chikawe.

 

In his response, Mr Chikawe said the investigation was still going on. “The investigation is yet to be completed and once completed the suspects would be arraigned if there would be sufficient evidence,” he told the Parliament.On the other hand, Mr Chikawe informed MPs that the government was planning to compile a report on the pending grand corruption cases and table it before the Parliament.

 

Responding to a question by Wawi MP (CUF), Mr Hamad Rashid Mohammed, Mr Chikawe said most of the cases have stalled at the Office of the Director of Public Prosecution (DPP). In his question, Mr Hamad referred to the statement by the Prevention and Combating of Corruption Bureau (PCCB) chief, Dr Edward Hosseah, during a seminar for MPs in Dar es Salaam that the anti-graft watchdog has completed many investigations but the files are still pending at the DPP’s office.Despite admitting the delays, the minister pledged to bring the report before the end of the ongoing Parliamentary session in Dodoma.

 

Meanwhile, the parliamentary committee on Justice and Constitutional Affairs will conduct a public hearing tomorrow to collect views on the 2011 Constitutional Review Bill.According to the Parliament’s schedule of activities, MPs will only have two day to debate the crucial 2011 Constitution Review Bill, which has been scheduled for tabling on April 18.The Speaker of the National Assembly, Ms Anne Makinda, told MPs that the hearing would be conducted in Dar es Salaam and Dodoma, urging stakeholders to attend and present their views.

 

“I urged all stakeholders to show up for the hearings at Karimjee Hall in Dar es Salaam and Pius Msekwa hall in Dodoma. We have opted for two different venues due to the importance of the issue,” Ms Makinda said.
According to the minister for Justice and Constitutional Affairs, Ms Celina Kombani, the government would conduct campaign, jointly with non-governmental organisations, to educate the public on the current constitution to enable them present informed views.

 

Ms Kombani was responding to a question by Special Seats MP (CCM), Ms Fakharia Shomar Khamis, who wanted to know plans by the government to educate the public on the new bill.

 

In what appears to be the legislator’s quest for the public involvement in the process, Civic United Front (CUF) MPs, Mr Habib Mnyaa (Mkanyageni) and Mr Mohammed Ibrahim Sanya (Mji Mkongwe) challenged the Speaker over the exclusion of the Parliament office in Zanzibar as a venue for the public hearing.

 

“Honourable Speaker even the Zanzibaris have the same need to participate in the planned public hearing, since the Constitution is a union matter. Why has the Zanzibar office not been involved?” queried Mr Sanya.
In her response, Ms Makinda said the Zanzibar office has been asked to mobilise people to come over to Dar es Salaam for the hearing.

Vijana CHADEMA watikisa Bunge

Tuesday, April 19th, 2011

WABUNGE machachari vijana wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) jana waliwasha moto bungeni, huku wakiilazimisha serikali na Bunge kuchukua hatua za haraka kujinusuru.

 

Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, alimbana vilivyo Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, akidai waziri huyo amelidanganya Bunge, huku Mbunge wa Ubungo, John Mnyika, akiibana serikali juu ya ufisadi wa Kagoda.

 

Wakati Lissu alikuwa tayari kuthibitisha kauli yake pale pale, kama kanuni zinavyotaka, Spika wa Bunge, Anne Makinda, aliingilia kati kumnusuru Ngeleja, akataka mbunge huyo awasilishe hoja yake kwa maandishi kuthibitisha uongo wa waziri Ijumaa wiki hii badala ya jana.

 

Hata hivyo, Lissu alipinga uamuzi huo, akitaka kutetea kauli yake na kuthibitisha uongo wa waziri jana hiyo hiyo, bila mafanikio.

 

Lissu hakuridhika na majibu ya Ngeleja yaliyotokana na swali lake la nyongeza.

 

Katika swali hilo, Lissu alitaka kujua hadi sasa ni wananchi wangapi wameondolewa katika kata za Mang,onyi, Ikungi na Mhitiri ili kupisha kampuni ya uchimbaji madini ya Shanta Mining Co. Ltd iliyopewa leseni ya kutafiti dhahabu katika jimbo lake.

 

Vile vile, alitaka kujua kiasi cha pesa walicholipa; kwanini wamejenga uwanja wa ndege, na kwanini kampuni hiyo ilitwaa maeneo mengine kwa nguvu.

 

Waziri Ngeleja alijibu kwa kifupi, akisema kampuni hiyo haijachukua maeneo hayo kwa nguvu, na akaongeza kuwa hata mwaka 2008 alifanya ziara na kushuhudia hali hiyo.

 

Ndipo Tundu alisimama na kutaka kuuliza swali la nyongeza, lakini Makinda alikataa, Lissu akaomba mwongozo wa Spika.

 

Tundu aliposimama, alisema katika majibu yake Ngeleja ni mwongo; na akataka atoe ushahidi kuthibitisha uwongo wa waziri.

 

Hata hivyo, Spika Makinda alimtaka Tundu Lissu kuandika maelezo yake, ili Ngeleja ajibu, na kwamba atafikisha maelezo hayo kwenye vyombo vyake ili wayapitie na kutoa majibu bungeni.

 

Hali hiyo ilimlazimu Tundu kusimama tena na kupambana na Spika kwa kutumia kanuni za Bunge, akihoji iweje Mbunge anapotoa madai kama hayo atakiwe kuthibitisha papo hapo lakini yeye anaambiwa aandike.

 

Akijibu hoja hiyo, Makinda alisema kutokana na muda mchache uliopo, hawezi kuruhusu malumbano hayo Bungeni kwani yatamaliza muda wa maswali na majibu.

 

Alisema mazingira yaliyotokea kwa Tundu, yanafanana na tukio la Mbunge mwingine wa CHADEMA wa Arusha Mjini, Godbless Lema wa Arusha Mjini, ambaye katika mkutano wa Bunge uliopita, alitaka kujua hatua ambayo mbunge anaweza kumchukulia kiongozi mkuu kama Waziri Mkuu iwapo amelidanganya Bunge.

 

Ilikuwa mara baada ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda kutoa kauli ya serikali kuhusu maandamano na mkutano wa CHADEMA, ambayo polisi waliyasambaratisha na kuua watu watatu.

 

’’Jamani tusome vizuri kanuni. Hili ni kama tukio la Lema ambalo nitalitolea majibu kwenye mkutano huu. Sio lazima utoe maoni sasa hivi ndani ya Bunge.

 

“Ninamuagiza Tundu aniandike na Ngeleja atajibu, nitapeleka kwenye vyombo vyangu ambako wanaweza kuwakutanisha Lema na Ngeleja na Bunge kusomewa uamuzi Ijumaa. Huo ndio utaratibu,” alisema Makinda.

 

Hata hivyo hatua hiyo haikumridhisha Tundu Lissu ambaye akiwa nje ya Bunge alisema Spika ana nia ya kuwalinda mawaziri wanapobanwa bungeni.

 

Kwa upande wake, Mnyika aliibua upya suala la ufisadi wa Kampuni ya Kagoda, inayodaiwa kuchota mabilioni ya fedha katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), mali ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ambalo serikali imekuwa anaogopa kulijadili.

 

Mara kadhaa huko nyuma, viongozi waandamizi serikali wamesema kwamba ”kagoda hakamatiki” na kwamba ”hafahamiki,” huku taarifa zikionyesha kuwa ufisadi huo ulifanyika katika mazingira ya kisiasa yanayodaiwa kukinufaisha Chama Cha Mapinduzi (CCM).

 

Baadhi ya watu wanaodaiwa kuchota pesa hizo ni watu wazito ndani ya CCM na mfumo wa utawala nchini.

 

Ufisadi huo uliibuliwa Bungeni na aliyekuwa Mbunge wa Karatu, Dk. Willibrord Slaa, katika Bunge liliopita. Dk Slaa ni Katibu Mkuu wa CHADEMA.

 

Jana Mnyika aligusia suala hilo wakati akiuliza swali la nyongeza, akitaka kujua kauli ya serikali lini itakamilisha uchunguzi kuhusu kampuni hiyo ya Kagoda na kuwachukulia hatua wahusika.

 

Akijibu swali hilo kwa kifupi sana, Waziri wa Nchi Ofisi Rais (Utawala Bora), Mathias Chikawe, alisema serikali bado inaendelea na uchunguzi wa tuhuma dhidi ya kampuni hiyo.

 

Hata hivyo, jibu hilo lilionekana kutowaridhisha wabunge wengi kwani zaidi ya wabunge kumi walisimama kutaka kuuliza maswali ya nyongeza.

 

Akiuliza swali lingine la nyongeza, Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid (CUF), alihoji kuwa kwa kuwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa,(TAKUKURU) Dk. Edward Hosea, alisema tatizo la kesi ya ufisadi mkubwa kama wa Kagoda ni DPP, hivyo alihoji kama Serikali iko tayari kutoa taarifa Bungeni kuonyesha kesi zilizokwama kwa DPP.

 

Akijibu swali hilo, Waziri Chikawe alisema Serikali ipo tayari kutoa taarifa hiyo bungeni na itafanya hivyo katika mkutano huu wa tatu wa Bunge unaoendelea mjini hapa.

 

Kashfa ya Kagoda ambayo ilipata kulitikisa Bunge miaka mitano iliyopita, limekuwa likipigwa danadana na Serikali kwa sababu za kisiasa.

 

Kampuni ya Kagoda ilikwapua jumla ya dola za Kimarekani 30,732,658.82 (Sh. 40 bilioni) katika Akanuti ya Madeni ya Nje (EPA), ndani ya BoT. Fedha hizi na nyingine zipatazo Sh. 73 zilichotwa katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2005.

 

Taarifa zinaonyesha kuwa ni Yusuf Manji aliyedhamini Kagoda kufungua akaunti katika tawi la CRDB Benki la Holland jijini Dar es Salaam ambako mabilioni ya shilingi yalipitia.

 

Serikali imekuwa ikikana kufahamu wamiliki wa Kagoda na kwa zaidi ya miaka mitano sasa imekaa kimya juu ya wizi wa kampuni hiyo.

 

Aidha, serikali imekuwa ikijikanyaga kuhusu wizi huu. Aliyekuwa Waziri wa Fedha, Zakia Meghji, aliwaandikia maodita wa kampuni ya Deloitte & Touche ya Afrika Kusini akisema, fedha za Kagoda zilitumika kwa “kazi za usalama wa taifa.”

 

Katika barua yake ya Septemba 15, 2006, Meghji anasema, “Kama unavyofahamu vema, mamlaka ya serikali huwa na siri, vilevile haja ya kugharamia matumizi ya busara. “Kwa hiyo… malipo ya dola 30,732,658.82 za Marekani yaliyofanywa na BoT kwa Kagoda Agriculture Limited, yaliidhinishwa na serikali kugharamia matumizi yake nyeti na ilikuwa lazima kuchukua hatua hii ya kudumisha usiri huu.”

 

Hatua hii inaleta maswali mengi kuliko majibu; yakiwa ni pamoja na iwapo Manji na wakwapuaji wa Kagoda ndio hasa wanaitwa “Usalama wa Taaifa.”

 

Baadaye jana Mnyika alitoa tamko kwa vyombo vya habari likisema:

 

“Itakumbukwa kwamba Kagoda inatuhumiwa kuchota jumla ya dola za Marekani 30,732,658.82 (Sh. 40 bilioni) katika Akanuti ya Madeni ya Nje (EPA) katika Benki Kuu (BoT) mwaka 2005.

 

“Serikali imekuwa ikijichanganya kuhusu ufisadi wa Kagoda; mathalani tarehe 15 Septemba 2006 Waziri wa Fedha wa wakati huo Zakhia Meghji aliandika barua kwa wakaguzi wa mahesabu wa kampuni ya Deloitte & Touche ya Afrika Kusini kuwa fedha za Kagoda zilitumika kwa kazi ya usalama wa taifa na kutaka usiri na busara katika ukaguzi wa mahesabu ya kampuni hiyo. Baadaye Waziri Meghji alifuta barua hiyo.

 

“Nyaraka mbalimbali zinaonyesha kwamba cheti cha usajili wa Kagoda kilichotolewa na ofisi ya Wakala wa Usajili wa Leseni za Biashara na Makampuni (BRELA) kinaonyesha Kagoda ilisajiliwa 29 Septemba 2005.

 

“Mpaka sasa siri za ufisadi wa Kampuni hiyo na wa kampuni zingine zilizohusika kwa wizi wa Kagoda zimebaki kwa Rais Jakaya Kikwete na wajumbe watatu wa timu uliyoiunda wakati huo ikiwemo idadi na majina ya watuhumiwa wanaodaiwa kurejesha sehemu ya fedha.

 

“Wakati serikali imekuwa ikieleza kwamba haiwajui wamiliki wa Kagoda; taarifa mbalimbali zimekuwa zikimtaja Rostam Aziz (Mb) na wengine.

 

“Baadhi ya vyombo vya habari vimewahi kuandika kwamba Wakili Bhyidinka Sanze wa Kampuni ya mawakili ya Malegesi (Malegesi Law Chambers) ya Dar es Salaam katika maelezo yake kwa Kamati ya Rais ya kushughulikia wizi kwenye akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) alikiri kwamba alishuhudia mkataba wa Kagoda na mikataba mingine iliyohusu ufisadi huo.

 

“Wakili huyo alieleza kwamba mkataba huo ulishuhudiwa na Caspian Construction Limited (inayomilikiwa na Rostam Aziz) iliyopo Dar es salaam na kwamba alielezwa kuwa fedha hizo ni kwa ajili ya kuiwezesha CCM kugharamia uchaguzi na kwamba maelekezo hayo yalitolewa kwa aliyekuwa gavana wakati huo (marehemu Daudi Balali) na Rais wakati huo Benjamin Mkapa.

 

“Hata hivyo, pamoja na serikali kwa wakati wote kuendelea kusisitiza kutowajua wamiliki wa Kagoda; Taarifa za hivi karibuni zimemtaja mfanyabiashara Yusuph Manji kupitia kampuni ya familia yake ya Quality Finance Corporation Limited (QFCL) anadaiwa na serikali kurejesha fedha za Kagoda.

 

“Katika mazingira haya ya utata ndio maana natoa kauli ya kuitaka serikali kutoa tamko la kina kuhusu kashfa hii ya Kagoda.”

 

Swali la msingi liliulizwa na Mbunge wa Viti Maalum Pudenciana Kikwembe (CCM), kuhusu rushwa, akitaka kujua Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba lengo la taifa katika kupambana na rushwa linafanikiwa.

 

Waziri Chikawe akijibu swali hili alisema kwa kuwa watoaji na wapokeaji wa Rushwa ni wananchi wenyewe, hivyo kila mmoja anapaswa kuwa askari.

 

“Vita hii ni yetu sote, ninawaomba viongozi wote wa serikali, siasa na dini na jamii kwa ujumla, kukemea rushwa kila wanapopata nafasi ya kufanya hivyo,” alisema Spika.

 

Wakati huo huo, moto juu ya mjadala wa Katiba mpya uliwaka jana Bungeni, huku baadhi ya wabunge wakitaka muswada wa serikali unaopelekwa Bungeni uahirishwe.

 

Aliyeibua hoja hiyo ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA), akisema wananchi wanahitaji kupewa muda wa kujadili suala hili kabla halijatungiwa sheria.

 

Zitto alisema ni wabunge wapewe fursa ya kuwaelimisha wananchi wao.

 

Lakini Waziri wa Katiba na Sheria, Celina Kombani, alisisitiza kuwa muswada huo utawasilishwa kama ilivyopangwa.

 

Akijibu swali bungeni jana, Kombani alisema kinachofanyika sasa si kupitisha Katiba Mpya bali kuangalia jinsi ya kuunda tume itakayosimamia kutungwa kwa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Mpya.

 

Alisema sheria hiyo, pamoja na mambo mengine, ndiyo itakayoanzisha tume itakayoratibu zoezi la utungwaji wa Katiba Mpya.

 

Alisema muswada huo umekamilika na utawasilishwa katika mkutano huu wa Bunge kwa hatua zaidi.

 

Waziri Kombani ambaye alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum (CUF) Fakharia Shomar Khamis, alisema muswada huo sanjari na kuainisha majukumu ya tume, utaanisha jukumu la utoaji elimu kwa wananchi kuhusu katiba inayotumika sasa.

 

“Watu wanapotosha kwamba Bunge limekuja kupitisha muswada wa Katiba Mpya. Nimeona kwenye kongamano na watu wengine wakijadili. Mkawaambie wananchi hatupitishi katiba mpya sasa,” alisema Kombani.

 

Kwa mujibu wa Kombani, katika utoaji elimu, Serikali itashirikiana na mashirika yasiyo ya kiserikali.

 

Alisisitiza kuwa serikali imeona kuna umuhimu wa kutoa elimu juu ya katiba ya sasa ili wawe katika nafasi nzuri ya kuchangia mawazo ya kuanzishwa kwa Katiba Mpya.

 

Katika swali lake la msingi, mbunge huyo alihoji kama Serikali haioni umuhimu wa kutoa elimu juu ya Katiba ya sasa ili wananchi waweze kuchangia mawazo ya kuanzishwa kwa Katiba Mpya.

 

Hata hivyo, wadau wa katiba, wakiwamo wanasheria, wanasiasa na wasomi kadhaa nchini, wanadai kuwa sheria inayotarajiwa kutungwa kwa muswada huu haikidhi matakwa, na haiendani na mahitaji ya Katiba mpya inayotakiwa.

 

Hoja kuu ambayo imekuwa ikijengwa kwa muda mrefu na wanazuoni, ni kwamba uhalali wa Katiba unatokana na uhalali wa mchakato wa kuitengeneza, na kwamba kwa staili hii ya harakaharaka ya serikali kutunga sheria inayolalamikiwa, wananchi watashindwa kushiriki kutunga katiba yao.

 

Wadau wengi wanadai muswada huu hauna maslahi kwa taifa, bali unalenga kulinda maslahi ya kikundi kinachotawala, na kunyamazisha wakosoaji wake.

 

Wanasiasa wapinga muswada wa kurekebisha katiba

Tuesday, April 12th, 2011

Baadhi ya washiriki wa kongamano la pili la katiba lililofanyika katika Ukumbi wa Nrumah Chuo Kikuu cha Dar es Salaam jana, wakifutila mada mbali mbali wakati wa kongamano hilo. Picha na Joseph Zablon.

 

 

Elias Msuya na   Freddy Azzah
WAKATI serikali ikijiandaa kuwasilisha Muswada wa Marekebisho ya Katiba bungeni wiki ijayo, wanasiasa na wasomi wameupinga wakisema utawabana wananchi.Hata hivyo, wawakilishi wa CCM na UDP walionja joto la jiwe na kulazimika kukatisha hotuba zao, baada ya kuzomewa na washiriki wa Kongamano la kujadili Muswada wa Marekebisho ya Katiba lililofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam jana.

 

Viongozi wa vyama vya siasa vya upinzani na wanasheria walioshiriki kongamano hilo walipinga mfumo utakaotumiwa kwa maelezo kuwa unawanyima wananchi haki.Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, ambaye alishiriki katika kongamano hilo, alisema chama chake hakioni nia njema ya serikali katika kuunda katiba mpya, hivyo wataipinga bungeni na nje ya bunge. Chama hicho kimeapa kutumia maandamano kwa kile wanachokiita nguvu ya umma kuupinga muswada huo kama utapitishwa na Bunge kuwa sheria.

 

“Najua watu wanazungumzia amani, lakini tutaheshimu amani kama inajali maslahi ya wananchi…Tutapinga muswada huo bungeni na kama Bunge litaendeshwa kwa ushabiki, tutarudi kwa wananchi na majibu mtayaona,” alisema. Serikali inatarajia kuwasilisha muswada huo wiki ijayo bungeni, kwa hati ya dharura ili uweze kupitishwa.

 

Akihutubia taifa, Rais Jakaya Kikwete juzi alizungumzia suala la katiba mpya ikiwamo muswada huo.
Naye Mwakilishi wa Chadema katika kongamano hilo, Mabere Marando alisema muswada huo umedhihirisha kuwa Serikali haikuwa na nia ya kuleta katiba mpya bali kuifanyia marekebisho katiba ya sasa.

 

Alikosoa kifungu cha tano cha muswada huo kinachompa uwezo Rais kuunda Tume na kuipa hadidu za rejea.
“Kifungu cha tano kinampa uwezo Rais ambaye ni Mwenyekiti wa CCM akishauriana na Rais wa Zanzibar kuunda tume na kuteua wajumbe na kuwapa hadidu za rejea. Yaani viongozi wawili wa CCM ndiyo wawateue Watanzania Tume ya Katiba,” alisema Marando.

 

Mwakilishi NCCR
Naye Mkurugenzi wa Sheria wa Chama cha NCCR Mageuzi, Dk Sengondo Mvungi, alisema chama chake kimesikitishwa na muswada huo na kwamba watakaa na vyama vingine ili wapeleke hati ya marekebisho ya muswada kabla ya kujadiliwa bungeni.

 

“Nimepokea ushauri kutoka kwa Dk Slaa kwamba sasa inabidi tukae mkao wa uanaharakati ili kupinga muswada huo. Kwanza tutapeleka ‘schedule of amendment’ (hati ya marekebisho) ya muswada kabla haujajadiliwa,” alisema Dk Mvungi. Dk Mvungi alisema kuwa kilio cha Watanzania tangu mfumo wa vyama vingi uanzishwe nchini mwaka 1992 ni kuwa na katiba mpya, siyo marekebisho ya Katiba.

 

Mwakilishi wa CUF
Naye Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Julius Mtatiro, alisema  chama chake kimesikitishwa na muswada huo na kuonya kuwa, kama serikali itaendelea nao Tanzania itaingia kwenye machafuko. “Tulipomsikia Rais Kikwete akitoa hotuba kwa tabasamu mwishoni mwa mwaka jana, tulidhani ana nia njema, kumbe muswada huo hauna hata chembe ya tabasamu. Umejaa vitisho vya kila aina, vitisho hivyo vya nini?” alihoji Mtatiro.

 

Mwakilishi  CCM azomewa
Hata hivyo, hali ya hewa katika kongamano hilo ilichafuka baada ya Mwakilishi wa CCM, Prince Bagenda kupanda jukwaani na kuanza kutoa maoni ya chama chake ambapo washiriki wa kongamano hilo walianza kumzomea kila alipoendelea kuzungumza.

 

Bagenda alikiri kwamba hoja ya Katiba haikuwa ya CCM, lakini akasema CCM ilikubali kwa kuwa Serikali huongozwa kwa maoni ya wananchi. Hata hivyo, Bagenda aliwakera watu aliposema suala la katiba haliji hivi hivi tu, bali wananchi wanapaswa kudai. “Msifikiri kila kitu mnapewa tu, lazima mdai,” alisema Bagenda huku akizomewa na washiriki wa kongamano hilo. Baadaye alishindwa kuendelea kutokana na kuzomewa licha ya Msimamizi wa kongamano hilo, Dk Kitila Mkumbo, kujaribu kuwatuliza watu bila mafanikio.

 

Cheyo wa UDP
Hali ilikuwa hivyohivyo kwa Mwenyekiti wa UDP ambaye pia ni Mbunge wa Bariadi Mashariki, John Cheyo, ambaye alishindwa kuendelea na mada yake baada ya watu kuanza kumzomea. Cheyo alisema kuwa muswada huo bado haujawa sheria kwa hiyo hakuna haja ya kuulalamikia sana na kwamba ingawa watu wanaupinga kinachotakiwa kuzingatiwa ni amani.

 

Jaji Samata
Jaji Mkuu Mstaafu Barnabas Samata, alisema katiba ya sasa ina upungufu zaidi ya 100 na baadhi ya upungufu huo kuwa ni pamoja na katiba hiyo kutomhusisha Mungu. “Nchi yetu imetajwa na Katiba kuwa ni ‘circular’ (isiyo na dini) ila watu wake wana dini. Kuwa circular maana yake nchi hiyo iko kinyume na Mungu. Hakuna hata kifungu kimoja kinachomtaja Mungu, lakini kwenye wimbo wa Taifa tumemtaja Mungu mara nyingi tu,” alisema Jaji Samata.

 

Upungufu mwingine ni pamoja na Katiba kutoenzi waasisi wa taifa, Rais kuwa sehemu ya Bunge, kupewa madaraka makubwa, Bunge kuwa na nguvu kubwa, matokeo ya urais kutopingwa mahakamani, Rais kutokuwa na kikomo cha uteuzi wa mawaziri, nchi kutokuwa na itikadi maalumu ya siasa na kutokuwapo kwa mahakama ya Katiba.

 

Jaji Samata alitaka pia, kabla ya kuandikwa kwa katiba mpya vyama vya siasa vyote vikae na kupanga namna misingi ya siasa itakavyokuwa ili kuwezesha nchi kuongozwa kwa misingi ya katiba na siyo utashi wa kiongozi mwenyewe.Pia katika katiba inayotarajiwa kuandikwa, alisema rais asiwe sehemu ya Bunge ila ashirikishe tu pale panapohitajika ikiwa ni pamoja na kusaini sheria na kuhutubia Bunge akiwa kiongizi wan chi na siyo sehemu ya Bunge.

 

“Hali hiyo itatoa uhuru zaidi kwa bunge kufanya shughuli zake, lakini pia utatoa tatizo la mihimili ya dola kutoingiliana katika utendaji wake wa kazi,” alisema Jaji Samata.

 

Francis Kiwanga
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Biandamu, Francis Kiwanga, ambaye aliukosoa muswada huo akisema kuwa rais amepewa madaraka makubwa mno katika kuunda Tume ya Katiba.
Alisema sehemu ya tatu ya muswada huo inampa madaraka rais kuunda tume, kuunda baraza la katiba na kutoa hadidu za rejea. “Rais ni zao la katiba, hawezi kutengeneza Katiba chafu awape wananchi. Wananchi wameporwa mamlaka kwa kumfanya rais kama chombo cha kutengeneza Katiba,” alisema Kiwanga.

 

Profesa Shivji
Naye Profesa Issa Shivji alisema muswada huo una matatizo ya lugha, muundo, mantiki pamoja na kisiasa.
“Ukiusoma kwa umakini utaona unazungumzia mapitio ya katiba hii tuliyonayo na siyo kuandikwa kwa katiba mpya kama tunavyotaka,” anasema Profesa Shivij.Alisema maelezo ya muswada huo juu ya kuundwa kwa tume ya kukusanya maoni, kuundwa kwa Bunge la katiba na nani anayepaswa kukabidhiwa ripoti ya tume iliyokusanya maoni, vifungu vyote hivyo vina upungufu.