Posts Tagged ‘serikali’

The Constitutional Review Act, 2011

Thursday, July 28th, 2011

RAI YA JENERALI:Hatari ya vurugu inatoka kwa watawala, Slaa asiwape kisingizio

Thursday, June 9th, 2011

Na Jenerali Ulimwengu

 

KATIKA kipindi hiki tunapoikazania Serikali ya Rais Jakaya Kikwete isifanye mchezo na suala la Katiba, tunalo jukumu la kutuliza akili zetu na kupima kwa kina kila tunachokisema na kukiandika.

 

Nasema haya kwa sababu naona kama tunalo tatizo linalotokana na Serikali yetu kuonekana kama vile haina msimamo kuhusu suala hili kubwa na zito. Hakuna dalili za wazi zinazoonyesha kwamba Baraza la Mawaziri limeketi na kulijadili kwa undani na kupata msimamo wa pamoja, na wala hakuna dalili kwamba mkuu wa Serikali hiyo, Rais Kikwete amewapa watu wake maagizo kuhusu nini wafanya na nini waseme kuhusu mada hii ya Katiba.

 

Kinachojitokeza ni taswira ya kuparaganyika kwa mawazo na kutokuelewana miongoni mwa wale wanaotarajiwa kutuongoza. Kwa bahati mbaya, ingawaje sasa naamini watakuwa wamegundua kwamba walichokifikiria kuwa kitu rahisi, ni kigumu kweli kweli na wanatakiwa wajiandae kukishughulikia kwa umakini mkubwa kuliko huo walioudhihirisha hadi sasa.

 

Ningependa nirejee jambo ambalo nimekuwa nikilishadidia kwa muda mrefu kidogo: Suala la Katiba mpya limeshika kasi isiyokuwa ya kawaida, na wala haliwezi kuondoka kirahisi. Linahitaji kufanyiwa kazi itakayowaridhisha wananchi, na hiyo kazi haiwezekani ikafanyika ila kwa kuwahusisha wananchi kwa kiwango kikubwa kinachowezekana.

 

Ukweli ni kwamba, hata kama hatukuwa tumezowea hili, hivi sasa wananchi wanataka mabadiliko makubwa katika maisha yao, na wanataka kuanza na Katiba watakayoiandaa wenyewe.

 

Ni kwa nini wananchi wamefikia kiwango hiki cha utashi, mimi binafsi sina jibu la haraka, na kila mtu anaweza kuwa na maoni yake. Lakini naamini kwamba wananchi wengi wameanza kung’amua kwamba mambo hayaendi kama ambavyo yanatakiwa yaende.

 

Wanayaona maisha yao yakiwa hayana matarajio tena. wanaona hali zao za kiuchumi na kijamii zikizidi kuzorota. Wanaona maisha bora waliyoahidiwa kama ni mzaha wamechezewa. Wanawaona watawala wao kama waongo na wanafiki, wasiojali, wala rushwa na wauza nchi. Hawaamini lo lote linalosemwa na watawala kwani wamekwisha kudanganywa mara nyingi.

 

Sasa wamehamanika na wanataka mabadiliko, tena wanataka mabadiliko makubwa.

 

Nimekuwa nikifuatilia kwa kiasi fulani maandamano na mikutano ya viongozi wa CHADEMA katika mikoa ya Kusini, na nimekuwa nikiangalia maelfu ya watu wanaoshiriki katika maandamano hayo na mikutano hiyo. Ningekuwa mtawala ningeshitushwa na mikusanyiko ile kwa sababu ningetambua kwamba inabeba ujumbe mzito kwangu.

 

Ujumbe unaotoka katika maandamano yale na mikutano ile ni kwamba wananchi wamechoka. Ukiona kaumu ya watu kama tuliyoiona katika miji midogo na ya ‘pembezoni’ kama Sumbawanga wanaandamana na kukaa mkutanoni wakisikiliza kama watotot wa shule wanavyokaa darasani kumsikiliza mwalimu, unajua kwamba kuna kitu kimebadilika katika jamii ya Watanzania.

 

Lakini papo hapo ningependa kutoa angalizo. Kama nilivyowahi kuandika huko nyuma, hii si mara ya kwanza tunashuhudia hamaniko la aina hii la kutaka mabadiliko. Nimeandika kwamba tuliwahi kuona, hapa nchini, hamasa walizozua wanasiasa kama Chistopher Mtikila na Augustine Mrema wakati ule. Watu wengi waliwachukulia hawa kama wakombozi wao. Baadaye bila shaka walikuja kugundua kwamba matumaini yao yalikuwa yamegonga mwamba.

 

Lakini shauku ikiisha kujengeka kwamba hali iliyopo haifai na ni lazima ibadilike, shauku hiyo haiishi kwa sababu manabii waliotarajiwa kufanya kazi ya ukombozi wamedondoka kando ya njia, bali shauku hiyo huhamishwa na jukumu la ukombozi likatafutiwa manabii wengine. Na kwetu ndivyo ilivyokuwa.

 

Kikwete alipoingia madarakani mwaka 2005 shauku hiyo ilikuwa imehamishiwa kwake. Bila shaka mwenyewe atakuwa anakumbuka kwamba ilifika mahali wakati wa kampeni ndani ya CCM ikasemwa kwamba hata kama CCM wasingemchagua yeye kuwa mgombea, angepata kuwa rais kwa kupitia chama kingine cho chote. Hayo yalisemwa na wana CCM na wanachama wa vyama vya upinzani pia.

 

Hili nalisisistiza kwa makusudi mazima: Hizi ni dalili za kuhamanika na kukata tamaa kwa Watanzania wengi. Na hali hii imekuwapo kwa muda mrefu toka utawala wa Rais Ali Hassan Mwinyi hadi ule wa Rais Benjamin Mkapa. Sasa inajirudia katika utawala wa Rais Jakaya Kikwete.

 

Wananchi wengi wanaona mkombozi wao mpya, nabii wao mpya, ni CHADEMA. Wanachosema katika lugha ya miili yao ambayo naiona kupitia televesheni na kupitia magazeti, ni kwamba wakipata fursa ya kupiga kura na uchaguzi ukawa “huru na wa haki” wanaweza (na uwezekano huo ni mkubwa) watapiga kura kuichagua CHADEMA.

 

Sasa, kama tunavyojua, uchaguzi mwingine ni mwaka 2015. Bado tunayo miaka minne hadi tupate fursa nyingine ya kupiga kura. Ni vyema kwa wale wanaotaka kufanya mabadiliko katika utawala wa nchi hii kwa njia mbali mbali wakautumia muda uliosalia kujiandaa kwa ajili ya uchaguzi huo, na wale wanaotaka kuiondoa CCM madarakani wafanye kampeni ya nguvu ya kuwahamasisha wapiga kura kimawazo lakini pia na kuwahamasisha wajitokeza siku ya kupiga kura ili watimize azima yao.

 

Ndiyo maana nilijikuta nikiwa na wasiwasi (wiki chache zilizopita) nilipomsikia Katibu Mkuu wa CHADEMA, Willbrod Slaa akizungumza kama vile anao mpango wa kufanya mabadiliko anayotaka kuyafanya kabla ya uchaguzi ujao. Aliposema kwamba kuiondoa serikali ya Kikwete kabla ya 2015 hautakuwa uhaini anaweza kuwa anasema kweli, kwani uwezekano huo upo.

 

Kwa mfano Bunge linaweza, katika mazingira mahsusi yaliyoainishwa na Katiba, likamshitaki Rais kwa kosa la kuidhalilisha Ofisi yake, na kama akikutwa na hatia likamvua madaraka. Hiyo imeandikwa katika Katiba tuliyo nayo hivi sasa, na wala halina haja ya kusubiri Katiba mpya. Ndiyo maana nasema kwamba anachosema Slaa ni cha kweli kwa maana ya vifungu vya Katiba ya Jamuhuri ya Muungano kama ilivyo leo.

 

Kinachonitia hofu ni kwamba napata hisia kwamba Slaa hakujikita katika vifungu vya Katiba, angalau maelezo niliyoyasoma hayakusema hivyo, jambo ambalo linaweza kuzaa tafsiri kwamba njia mojawapo inayofikiriwa ni kuung’oa utawala wa Kikwete kwa maandamano, kama ilivyokuwa Medani Tahrir.

 

Kama hivyo ndivyo alivyokusudia kusema Slaa, kuna tatizo. Tatizo hilo, kwa mtazamo wangu, linakuwa kubwa zaidi kwa kuangalia matukio ya siku hizi chache zilizopita.

 

Tatizo lenyewe si kwamba haiwezekani kuung’oa utawala uliopo kupitia maandamano na bado kitendo cha kuung’oa kikawa si uhaini. Nchi nyingi zimeshuhudia hilo likifanyika, ikiwa ni pamoja na Indonesia, Philippines, Georgia na sasa Tunisia na Misri. Kilichotokea katika nchi hizo ni mapinduzi ya umma uliosimama na kusema “Utawala huu sasa basi!” Ni mantiki ya mapinduzi kama hayo kwamba yanapofanikiwa walioyaongoza wanakwenda moja kwa moja Ikulu, lakini wakishindwa wanatiwa kitanzi.

 

Ni kwa jinsi hii akina Fidel Castro (Cuba) na Nelson Mandela (Afrika Kusini) walikwenda jela lakini hatimaye waliingia madarakani, lakini Pierre Mulele (Kongo) na Mahjoub (Sudan) walitiwa kitanzi.

 

Naamini kwamba Katibu Mkuu wa CHADEMA alitaka kupeleka ujumbe mzito kwa wakuu wa nchi, lakini kila siku ujumbe unaohusu mambo kama haya hauna budi uandaliwe kwa uangalifu na weledi mkubwa ili usije ukazaa tafsiri zaidi ya moja.

 

Ingekuwa vyema kama Slaa angeonyesha subira katika matamko yake. Hivi sasa watu wengi wanamwangalia kama “rais mtarajiwa.” Angechukua muda kujiandaa kwa umakini mkubwa, hasa wa kuyasoma matatizo ya nchi yetu na kufikiria njia mbali mbali za kuyakabili kuanzia na hili la Katiba ambalo sasa naamini kwamba iwapo atachaguliwa kuwa rais mwaka 2015 ( na nasema hili linawezekana kabisa), atalikuta bado lipo kwa sababu sioni dhamira ya kweli ya kulishughulikia.

 

Akijipa muda wa kujifunza zaidi na kukusanya maoni, na kujenga mitandao ya utafiti itakayowahusisha wataalamu wa kumshauri na kukishauri chama chake, akichukua muda kujadili matatizo ya nchi hii na makundi mbali mbali ya kijamii katika shughuli zao mbali mbali na wakamweleza matatizo yao; naye akajadiliana nao… atakuja kugundua kwamba hakuna muda wa kutosha kwa ajili ya maandalizi hayo.

 

Najua mara nyingi umefanyika uchokozi dhidi ya vyama vya siasa na wanasiasa wa upinzani. Uchokozi huo unafanywa makusudi ili kipatikane kisingizio na wapinzani waweze kushutumiwa kwamba ndio waliodhamiria kuvunja “amani na utulivu” na misemo mingine ya kuchekesha ukiangalia “amani na utulivu” vinavyotawala shughuli za chama-tawala.

 

Kwangu ni dhahiri kwamba kama kuna ghasia kubwa zitakazotokea nchini humu, zitaanzia katika vurugu zinazoendelea ndani ya chama hicho tawala. Hata hivyo, Slaa angejiweka mbali na kila kinachoweza kumfanya yeye ama chama chake waonekane, hata kama si kweli, kwamba wao ndio wanaochochea vurugu.

 

Naandika haya nikijua kwamba sasa kuna hamaniko ndani ya duru za watawala, kwa sababu wanajua wamepoteza nguvu za ushawishi na wanachokiona kwamba kinaweza kuwasaidia ni ushawishi wa nguvu, kama ambavyo wanaonekana kutumia mitulinga isiyokuwa na sababu yo yote alimradi tu waonyeshe kwamba wanazo nguvu, kama vile hatujui kwamba wanazo.

 

Katika kutapatapa wamewaingiza na wakuu fulani wa dini ambao nao sasa wanatoa ‘onyo’ kwa CHADEMA kama vile wamegeuka kuwa idara ya usalama ya serikali au wasemaji wa Jeshi la Polisi.

 

Hali hii inatisha, lakini si mpya. Imetokea kila mahali utawala ulipozeeka, ukapoteza njia, ukasahau hata asili yake, ukapuyanga na kubahatisha, ukababaisha na kubangaiza, ukayumba na kutetereka, ukatekwa na waporaji, ukaendelea kujitutumua kwa kuonyesha ukali wa kijeshi kumbe ndani ya roho yake kiini chake kilikwisha kugugunwa na mapanya-buku kwa muda mrefu. Utawala kama huo unao uwezo mkubwa wa kusababisha maafa kutokana na udhaifu wake.

 

Slaa akae chonjo, apunguze hisia, awe m-rais (presidential). Ajifunze zaidi, kwani kama bado ana nia ya kuwania urais mwaka 2015, kazi iliyo mbele yake ni kubwa. Akumbuke tu kwamba, Rais Jakaya Kikwete alikuwa na (angalau) miaka kumi ya kujiandaa kuwa rais, na hii kumi ni ile tunayoijua sisi.

 

Hata baada ya muda huo wa miaka kumi kupita, na hata baada ya miaka mitano ya kuendesha Serikali, inaelekea bado hajajifunza mambo mengi ya msingi kabisa yanayohusu uongozi na utawala. Slaa afanye hadhari, asije akawa vivyo hivyo.

 

Chanzo: Raia Mwema

 

Bajeti ya upinzani 2011 yafuta posho za wabunge

Thursday, June 2nd, 2011

Boniface Meena
KAMBI ya Upinzani bungeni imetaja vipaumbele sita vya bajeti yake mbadala ya mwaka wa fedha 2011/2012, ikitaka kufutwa kwa posho (sitting allowance), za vikao vyote vya serikali na wabunge.Vipaumbele hivyo vimetangazwa jana, ikiwa ni wiki moja kabla ya serikali kuwasilisha bungeni, Bajeti yake ya mwaka 2011/2012 itakayotangazwa Jumatano ijayo.

 

Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo ameshatangaza vipaumbele 12 vya Bajeti ya Serikali ambavyo ni mara mbili ya vile vya kambi ya upinzani.
Kambi hiyo ya upinzani bungeni imeeleza kuwa katika vipaumbele vyake itaweka msisitizo katika miundombinu, umeme, kuwezesha ukuaji wa sekta za uzalishaji na hasa ukuaji wa uchumi vijijini na kuimarisha utawala bora.
Imetaja kuimarisha usimamizi wa mashirika ya umma na kuboresha maendeleo ya rasilimali watu kwa kuwekeza kwenye ubora wa elimu nchini.

 

Akitaja vipaumbele hivyo mbele ya waandishi wa habari jana, Naibu Waziri Kivuli, Wizara Fedha na Uchumi, Christina Mughwai alisema dhamira ya bajeti hiyo mbadala ni kutoa unafuu wa kodi kwa wananchi maskini na kuhakikisha kuwa anayepaswa kuilipa anafanya hivyo kwelikweli.
Mughwai ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), alisema bajeti hiyo itasomwa bungeni na Waziri Kivuli wa Fedha na Uchumi, Zitto Kabwe.

 

Kuhusu miundombinu


Alisema kuwa bajeti hiyo itaweka msisitizo kwa barabara zote muhimu ambazo hazijaanza kujengwa, ili zianze kuanzia mwaka huu wa fedha wa 2011/2012.

 

Mughwai alisema pia wataweka msisitizo katika upanuzi wa bandari kwa kutumia ushirikiano wa Sekta Binafsi na Serikali (Public Private Partnership- PPP) pamoja na kuimarisha Bandari ya Mtwara.

 

Alisema katika eneo hilo, watasisitiza pia uboreshwaji wa Reli ya Kati ili iweze kufanya kazi ya kusafirisha mizigo na abiria kwa kiwango cha kuridhisha hadi hapo fedha za kujenga reli mpya zitakapopatikana: “Pia Shirika la Ndege la Taifa liongezewe mtaji wa kulifufua, ili liweze kujiendesha kibiashara na kwa ufanisi.”

 

Tatizo la umeme


Kuhusu umeme, Mughwai alisema bajeti ya kambi ya upinzani itapendekeza fedha zipelekwe kwenye miradi mitatu mikubwa na kwamba miradi hiyo ianze mara moja.

 

“Miradi hiyo ni umeme wa makaa ya mawe megawati 1,500 katika Migodi ya Mchuchuma, Ngaka na Kiwira, pia umeme wa gesi (Mtwara Gas Pipeline) megawati 300 kutoka Mtwara, Dar es Salaam hadi Mwanza,” alisema Mughwai.

 

Alisema kambi hiyo pia itapendekeza mradi kabambe wa kusafirisha na kusambaza umeme mijini na vijijini chini ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na Wakala wa Nishati Vijijini (Rea) ufanye kazi kwa nguvu zaidi.

 

Sekta ya uzalishaji


Katika eneola uzalishaji, Naibu Waziri huyo Kivuli wa Fedha na Uchumi alisema wanasisitiza kuboresha miundombinu, upatikanaji wa majisafi na salama ikiwa ni pamoja na kuongeza ubora wa bidhaa za kilimo: “Tutaelekeza rasilimali za kutosha kwenye kukuza uchumi vijijini.”

 

Utawala Bora


Katika kuimarisha utawala bora, alisema kambi yake inataka serikali itenge fedha za kutosha kuwezesha mchakato wa kuandika Katiba Mpya ili Watanzania wote waweze kushiriki katika mchakato huo.

Pia alisema wanataka kuanzishwe kitengo maalumu kwa ufisadi mkubwa (Serious Fraud Office) ndani ya Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) ili kuimarisha utawala bora.Mughwai alisema kuwa wanataka pia mfumo mpya wa kudhibiti mgongano wa maslahi, hasa kwa wanasiasa kutenganisha mgongano wa maslahi katika biashara zao.

 

Alisema wanataka kuanzishwa kwa ofisi ya bajeti ya Bunge ili kuweka uwazi zaidi kwenye Bajeti ya Serikali kwa kuwa hivi sasa wabunge hawahusishwi katika kuipanga: “Tunapendekeza itungwe Sheria ya Bajeti itakayowezesha kuanzishwa kwa Ofisi ya Bajeti.”

 

Maendeleo ya rasilimali watu

 

Waziri huyo Kivuli wa Fedha na Uchumi alisema katika maendeleo ya rasilimali watu, kambi yake inataka kuhakikisha watoto wanaomaliza kidato cha nne, wanapata mafunzo ya ufundi ili waweze kujiajiri wanaporudi vijijini.

 

“Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu inapata fedha za kutosha kutoka kodi ya uendeshaji ujuzi, robo tatu ya kodi hii ambayo inakwenda Hazina ibaki kwenye bodi ili kukidhi mahitaji ya mikopo. Kimsingi lengo la bajeti yetu katika elimu ni kupata elimu bora na si wingi wa majengo ya shule ama wanafunzi wanaomaliza shule.”

 

Naibu msemaji huyo alisema kuwa wapinzani wanataka kuanzishwa pensheni kwa wazee wote wenye umri zaidi ya miaka 60 na kuanzishwa kwa bima ya afya kwa wananchi wote.”Bima hii iwe ni ya lazima kwa watu wote, wafanyakazi na wasio wafanyakazi na ichangiwe na wananchi wenyewe pamoja na serikali,” alisema.

Usimamizi wa mashirika ya umma

 

Kuhusu usimamizi wa mashirika ya umma, alisema kambi ya upinzani inataka uanzishwe Mfuko wa Taifa wa Uwekezaji (National Investment Fund) kwa ajili ya kutoa mitaji kwa mashirika ya umma na mapato yake yatokane na asilimia ya faida za mashirika inayokwenda kwenye bajeti sasa.

 

Alisema kambi hiyo pia inataka kuanzishwa kwa Mamlaka ya Mafuta na kulibadili Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kuwa shirika la kibiashara la mafuta.Pia kambi hiyo inataka kupunguzwa bei ya mafuta kwa asilimia 40 na kupanua wigo wa kodi kwa kuweka lengo la kukusanya mapato ya ndani sawa na asilimia 20 ya pato la taifa.

 

Mughwai alisema kambi ya upinzani pia inataka pia kuangaliwa upya kwa mfumo wa utawala wa kodi akitolea mfano kampuni zinazofanya kazi nchini, lakini zimesajiliwa nje hali inayosababisha zilipe kodi katika nchi zilikosajiliwa na taifa kukosa mapato.

 

“Tunataka kodi inayoitwa ‘Presamptive Tax’ ifutwe kwa sababu inasababisha kampuni ndogo zisijisajili, hii husababisha ukwepaji wa kodi hasa katika sekta isiyo rasmi.Alisema mashirika ambayo serikali ina hisa yajisajili katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), ili ziweze kuuzwa.

 

Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2011/2012 itaelekezwa katika sekta za nishati, elimu, kilimo na mifugo. Sekta nyingine zitakuwa ni za miundombinu,Uvuvi, maendeleo ya viwanda, afya, maji, ardhi, nyumba na makazi, rasilimali watu, sayansi na teknolojia, huduma ya fedha na masuala mtambuka.

 

Chanzo:Mwananchi

Marando: Tunamtaka Rais mahakamani:PROFESA MAHALU KUANZA UTETEZI LEO

Tuesday, May 31st, 2011

James Magai na Tausi Ally

 
WAKILI Mabere Marando anayemtetea Profesa Costa Mahalu aliyekuwa na Balozi wa Tanzania nchini Italia, amesema ataiomba mahakama imlazimishe Rais Jakaya Kikwete kufika mahakamani kumtetea mteja mteja wake iwapo hatakubali kwenda kutoa ushahidi baada ya kuombwa kufanya hivyo kwa barua.Marando ametoa kauli hiyo wakati Profesa Mahalu na mwenzake Grace Martin wakianza kujitetea leo.

 

 

Mbali na utetezi wao binafsi, wanatarajia pia kuwa na mashahidi kadhaa wa kuwatetea akiwamo Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa pamoja na Rais Kikwete.Tayari Rais Mkapa amewasilisha mahakamani hapo hati yake ya kiapo akimtetea Profesa Mahalu na mwenzake kuhusiana na tuhuma zinazowakabili huku akibainisha kuwa yuko tayari kufika mahakamani iwapo italazimu.

 

 

Lakini hadi jana, Rais Kikwete alikuwa hajajibu barua aliyoandikiwa na Wakili Marando kwa niaba ya wateja wake wakimwomba akubali wa kufika mahakamani kuwatetea au kuwasilisha kiapo chake ambacho kitatumika kama ushahidi wa utetezi dhidi yao.

 

Marando alisema jana kuwa Rais Kikwete alikuwa hajajibu barua hiyo, lakini akasema ikiwa Profesa Mahalu atamaliza kujitetea pamoja na mashahidi wengine kabla Rais Kikwete hajakubali, wataiomba mahakama imkumbushe.

 

 

“Kama atakaidi hata baada ya mahakama kumwandikia, basi tutaomba kesi hiyo iahirishwe hadi mwaka 2016 (wakati atakapokuwa amemaliza muda wake wa urais) ili imlazimishe kuja kutoa ushahidi huo,” alisema Marando.

 

Mei 3, mwaka huu Wakili Marando alimwandikia barua Rais Kikwete yenye kumbukumbu namba MM/PCRM/2011/1 kupitia kwa Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo, akibainisha kuwa ni miongoni mwa mashahidi muhimu ambao wateja wao wamewaagiza wamwite.

 

 

Barua hiyo inabainisha kuwa umuhimu wa Rais Kikwete katika ushahidi huo wa utetezi unatokana na ukweli kwamba nyumba hiyo ya Ubalozi wa Italia ilinunuliwa wakati akiwa Waziri wa Mambo ya Nje na kwamba alikuwa na taarifa zote kuhusu mchakato wa ununuzi wake.

 

 

Mchakato huo, kwa mujibu wa barua hiyo ni pamoja na nguvu ya kisheria aliyopewa mteja wao ambayo ilisainiwa na Rais Kikwete wakati huo akiwa Waziri Septemba 24, 2004 pamoja na hotuba yake aliyoitoa Bungeni Agosti 3, 2004 akithibitisha kuwa ununuzi wa jengo hilo haukuwa na mushkeli wowote.

 

Pia barua hiyo inaweka wazi kuwa kuna barua nyingi tu ambazo Profesa Mahalu alimwandikia Kikwete akiwa waziri, pamoja na katibu mkuu wa wizara hiyo, ambazo anapaswa kuzitambua mahakamani wakati wa utetezi.

 

 

“Kwa hiyo tunaomba kwa unyenyekevu kabisa, uweke barua yetu hii mbele ya Mh. Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania; aisome na akueleze utujibu kama hana pingamizi kuja kueleza ukweli mahakamani. Kama muda wake hauruhusu, kulingana na ratiba zake za kitaifa, tunaomba aturuhusu tumwandalie kiapo (affidavit) kitakachoeleza yaliyotekea ili tukiwasilishe mahakamani badala ya kumwita yeye mahakamani”, inasisitiza barua hiyo na kuongeza kuwa hakuna kifungu cha Katiba kinachozuia Rais kuitwa kutoa ushahidi mahakamani.

 

Katika kiapo chake alichokiwasilisha mahakamani, Mkapa anamtetea Mahalu na akidai kuwa amefanya naye kazi kwa muda mrefu na anamjua kuwa ni mtu mwaminifu, mtiifu na mchakapakazi. Mkapa alieleza katika hati yake hiyo kuwa mchakato wa ununuzi wa jengo hilo ulifanyika wakati wa uongozi wake na kwamba alikuwa akijua kila kilichokuwa kikiendelea kuhusiana na ununuzi huo na kwamba ulifanyika kwa mujibu wa sheria.

 

 

Alifafanua kuwa mpango wa ununuzi wa jengo hilo ulikuwa ni utekelezaji wa sera ya serikali wa kuwa na majengo yake ya kudumu katika kila ubalozi kwa kununua au kujenga ikiwa ni njia ya kupunguza gharama za upangaji. Aliongeza kuwa serikali yake ilimpa Profesa Mahalu mamlaka yote kupitia nguvuya kisheria ya kusimamia na kutekeleza mchakato wa ununuzi wa jengo.

 

Mkapa alisisitiza kuwa kupitia utaratibu wa serikali, alikuwa akijua kuwa taarifa ya uthamini wa jengo hilo iliyofanywa na Wizara ya Ujenzi ilikuwa ni Dola za Marekani 3.0 milioni wakati Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, ilikadiriwa Euro 5.5 milioni: “Kupitia utaratibu wa serikali nilifahamu kuwa jengo hilo lilinunuliwa kwa gharama ya Dola za Marekani 3.0milioni sawa na Euro 3,098,741.40,” alisema Mkapa.Pia Mkapa alisisitiza kuwa alikuwa na bado anatambua taarifa ya serikali bungeni ya Agosti 3, 2004 iliyoeleza na kuthibitisha kuwa taratibu zote za ununuzi wa jengo hilo zilifuatwa kwa mujibu wa maelekezo ya serikali na kwamba dalali alilipwa kikamilifu.

 

 

“Kwa kipindi chote ambacho nimefanya kazi na Balozi Mahalu katika nafasi mbalimbali za utumishi wa serikali ameonyesha tabia thabiti na za dhati, uaminifu, utiifu, uchapakazi na ubora,” alisema Mkapa.

 

Alisema kuwa sifa hizo zilimfanya atunukiwe na Rais wa Italia, Tuzo ya Heshima ya Juu wakati wa kuadhimisha Siku ya Taifa hilo, muda mrefu baada ya kuwa ameondoka nchini humo.

 

Profesa Mahalu na mwenzake, Martin aliyekuwa Ofisa Utawala wa ubalozi huo wanakabiliwa na mashtaka hayo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakidaiwa kuhujumu uchumi kwa kuisababishia Serikali hasara ya Euro 2,065,827.60. Wanadaiwa kusababisha hasara hiyo kupitia mchakato wa ununuzi wa jengo la ubalozi huo, wakati wa utumishi wao.

 

 

Kutokana na mashtaka hayo, leo wanadiplomasia hao wanaanza kujitetea baada ya mahakama hiyo kuwaona kuwa wana kesi ya kujibu.Mahalu na Martin wanadaiwa kula njama na kutenda makosa hayo katika tarehe tofauti na katika maeneo tofauti huko Italia, likiwamo la kumpotosha mwajiri wao katika hati ya matumizi.

 

 

Miongoni mwa mashtaka hayo ni kwamba Septemba 23, 2002 huko Rome, washtakiwa wakiwa waajiriwa wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, walisaini vocha yenye namba D2/9/23/9/02 ikionyesha kuwa bei ya ununuzi wa jengo la ubalozi ni Euro 3,098,741.58, maelezo ambayo yalikuwa ni ya uongo na yenye nia ya kumdanganya mwajiri wao.

 

Chanzo:Mwananchi